Alhamisi 22 Oktoba 2026 - 10:00
Mkutano wa Awali wa Kongamano la Kimataifa la Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah Wafanyika Qum/ Nafasi Yake ya Kielimu, Kistaarabu na Kuitii Wilayat Vyaashiriwa

Hawza/ Mkutano wa awali wa kitaaluma wa Kongamano la Kimataifa la “Allamah Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah”, uliolenga kupitia upya nafasi na mchango wa shahidi huyo mtukufu katika medani ya kimataifa na ulimwengu wa Kiislamu, umefanyika mjini Qum, ukihudhuriwa na kundi la watu mashuhuri kutoka Hawza na vyuo vikuu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, likinukuu Shirika la Habari la ABNA, mkutano huo wa awali wa kitaaluma wa Kongamano la Kimataifa la Allamah Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah ulifanyika jana, Jumatano, tarehe 29 Mehr 1405 Hijria Shamsia, katika Jumuiya ya Ahlul-Bayt (a.s.) mjini Qum. Mkutano huo ulilenga kupitia upya nafasi na mchango wa shahidi huyo mtukufu katika medani ya kimataifa na ulimwengu wa Kiislamu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na kundi la watu mashuhuri kutoka Hawza na vyuo vikuu, akiwemo Ustadh Reza Ramazani, Katibu Mkuu wa Majma'u Ahlul-Bayt (a.s.); Sheikh Hussein al-Matouq, mjumbe wa Kuwait katika Baraza Kuu la Majma'u Ahlul-Bayt (a.s.); Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad al-Najdi, mwakilishi wa Hizbullah ya Lebanon mjini Qum; Dkt. Mohammad Mahdi Shariatmadar, aliyekuwa mshauri wa kitamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon; pamoja na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohammad Hassan Zamani, mshauri wa mkuu wa Hawza za elimu ya dini nchini Iran.

Washiriki hao walichambua vipengele vya utu wa Shahidi Nasrallah ambavyo havifahamiki sana, kwa kuzingatia fiqhi ya Muqawama, falsafa, usimamizi wa kimkakati na kuitii Wilayat al-Faqih.

Muqawama ni rehema yenyewe

Katika mkutano huo wa awali, Ustadh Ramazani alirejelea maelezo ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu watu mashuhuri, akisema: “Imam Shahidi alitumia neno ‘maktab’ (mfumo wa kimawazo na kimafundisho) kuwahusu watu wawili, na neno ‘jambo la kipekee’ kuwahusu watu wengine wawili. Miongoni mwa watu ambao aliwahusu kwa neno ‘maktab’ ni Shahidi Hajj Qassem Suleimani na Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah.”

Katibu Mkuu wa Majma'u Ahlul-Bayt (a.s.) alisisitiza kuwa: Shahidi Nasrallah alianzisha harakati ya kistaarabu, akiongeza kuwa fiqhi ya Muqawama katika uzoefu wa Shahidi Nasrallah ilikuwa mfumo wa kisasa wa utawala uliokuwa na vipengele vya kifiqhi, kimaadili, kimkakati na kitaasisi.

Aliongeza kuwa, katika fikra za Shahidi Nasrallah, Muqawama haukuwa mtazamo wa kijeshi pekee, bali ulipata maana katika maisha ya wananchi na uliambatana na kuzingatia uadilifu pamoja na kujenga uaminifu.

Siri ya ushindi ilikuwa katika kumtii Imam Khamenei

Sheikh al-Matouq, kwa upande wake, alizungumzia vipengele vya kielimu vya Shahidi Nasrallah, akisema kuwa hakuwahi kuacha kuhudhuria vikao vyake vya kielimu na vya Hawza. Alikuwa amehudhuria zaidi ya darsa 500 za bahth al-kharij fiqh kutoka kwa Imam Khamenei.

Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Majma'u Ahlul-Bayt (a.s.) aliashiria watu watatu mashuhuri walioathiri kwa kiasi kikubwa uundaji wa fikra za Shahidi Nasrallah, ambao ni Shahidi Muhammad Baqir al-Sadr, Imam Khomeini na Imam Khamenei.

Alisisitiza kuwa katika mkutano mmoja wa mwaka 2000, Shahidi Nasrallah alimbusu Imam Khamenei mkononi kwa makusudi, ili kuwafahamisha watu wote kuwa siri ya ushindi wote imo katika kutii Wilayat al-Faqih.

Kuwabadilisha Mashia kutoka kundi lililoonekana kuwa dhaifu na kuwa kitovu kikubwa cha nguvu

Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad al-Najdi, ambaye alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wengine katika mkutano huo wa awali, alisisitiza nafasi kuu na ya kipekee ya Sayyid al-Muqawama katika kuleta mabadiliko katika jamii ya Kishia nchini Lebanon.

Alisema kuwa Shahidi Nasrallah, kupitia malezi ya kijihadi na kuimarisha mwamko na utambuzi, aliwabadilisha Mashia kutoka kundi lililoonekana kuwa dhaifu na kuwafanya kuwa kitovu kikubwa cha nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mwakilishi wa Hizbullah ya Lebanon mjini Qum alirejelea kaulimbiu isemayo: “Sisi si watumishi wa Marekani na Israel, bali ni mabwana wa Wilaya.”

Alisisitiza kuwa jibu lao kwa Trump ni jibu lilelile alilolitoa Bibi Zainab (s.a.) huko Karbala, aliposema: “Hawa ni watu wauaji ambao wamewatawala.”

Shahidi Nasrallah alikuwa kiongozi aliyejenga taasisi na mwenye mtazamo wa mbele

Dkt. Mohammad Mahdi Shariatmadar, aliyekuwa mshauri wa kitamaduni wa Iran nchini Lebanon, alielekeza mazungumzo yake katika sifa za kipekee za kiutawala za Shahidi Nasrallah.

Alisema: “Tofauti na makatibu wakuu waliomtangulia ndani ya Hizbullah, Shahidi Nasrallah alikuwa kiongozi aliyejenga taasisi na aliyekuwa na mwelekeo wa kutekeleza mambo kwa vitendo, akiongozwa na tafiti na tathmini kuhusu mustakabali.”

Akizungumzia uandaaji wa mfumo wa fiqhi ya taasisi na miundo ya kiutendaji kwa kutegemea fatwa za Imam Khamenei, uliofanywa na Shahidi Nasrallah, alibainisha kuwa; shahidi huyo alikuwa na imani thabiti katika kutekeleza wajibu wa kidini kwa kufuata Wilaya.

Alisema kuwa Shahidi Nasrallah aliamini kwamba jambo lolote likitokana na uongozi, hata kama halijatolewa kwa njia ya amri ya moja kwa moja, ni wajibu wao kulitekeleza.

Kujitolea kila kitu kwa ajili ya kiongozi wa zama hizi

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohammad Hassan Zamani, mshauri wa mkuu wa Hawza za elimu ya dini, alichambua nguzo kumi za msingi za utii wa Sayyid al-Muqawama kwa Wilaya.

Akizungumzia vipengele vya utu wa Shahidi Nasrallah, alisema kuwa Imam Khamenei alitumia neno maktab kuwahusu watu wawili tu, ambao ni Shahidi Hajj Qassem Suleimani na Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah.

Akirejelea dua ya Shahidi Nasrallah kwa ajili ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, alisema kuwa katika mahojiano ya televisheni, shahidi huyo aliwahi kusema: “Mimi kila siku ninamuomba Mwenyezi Mungu achukue umri uliobaki kwangu na kwa familia yangu kwa pamoja, kisha auongeze katika umri wa Kiongozi mpendwa wa Mapinduzi.”

Alisema kuwa kauli hiyo inaonyesha kiwango cha juu kabisa cha mapenzi na kujitolea kwake kwa ajili ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi.

Zaidi ya makala 600 zimewasilishwa kwenye sekretarieti ya kongamano hilo

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Iskandari, Katibu wa Kongamano la Umana al-Rusul, alieleza mwanzoni mwa mkutano huo hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya kongamano kubwa la kuadhimisha nafasi ya kielimu ya Shahidi Nasrallah.

Alisema kuwa katika baraza la kitaaluma lililoundwa na taasisi za Hawza na za kielimu, watu saba walichaguliwa kutoka katika orodha ya wanazuoni na watu mashuhuri 100 kwa ajili ya kuandaliwa makongamano ya kuwaenzi, Allamah Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah alikuwa miongoni mwa waliowekwa katika nafasi za kipaumbele.

Aliongeza kuwa hadi sasa, zaidi ya makala 600 zimewasilishwa kwenye sekretarieti ya kongamano hilo. Kuhusu sehemu ya mahojiano, alisema kuwa miradi 20 imeainishwa, na inatarajiwa kuwa miradi 12 itakamilika na kuchapishwa katika mfumo wa vitabu.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Iskandari pia alizungumzia shughuli za kongamano hilo katika mikoa mbalimbali ya Iran, huku akibainisha kuwa shughuli tayari zimefanyika katika mikoa ya Khorasan, Fars na Isfahan.

Alisema kuwa mada saba zimechaguliwa na kuwasilishwa kwenye vyuo vikuu vyote vya huru, na kuanzia wiki ijayo, shughuli za kuandaa na kuendesha makongamano hayo zitaanza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha